Wagombea 10 ccm wapinga
matokeo ubunge Mwanza
By Charles Mseti
JUMLA ya wagombea10 kati
ya 20 walioshindwa kwenye kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika jimbo la
Nyamagana Jijini Mwanza, wameandika waraka mzito wa kupinga matokeo, yaliyompa
ushindi Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula.
Wagombea hao wameandika
waraka unaolalamikia matokeo ya uchaguzi huokwamba haukufanyika kwa haki na
huru kutokana na kutawaliwa na vitendo vya rushwa vilivyokuwa vikifanywa na
meya huyo.
Waraka huo ulioandikwa
na wagombea hao umetumwa kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdurlahiman Kinana na nakala
yake kutumwa kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Phillip Mangula, Mwenyekiti
wa chama hicho Mkoa wa Mwanza, Dk. Anthony Diallo, Katibu wa Mkoa, Miraji
Mataturu na Mkuu wa Mkoa, Magesa Mulongo.
Wagombea hao ni kati ya wanachama 20 wa CCM walijitokeza kuingia katika
kinyang’anyiro hicho akiwamo, Mabula ambaye alitangazwa mshindi baada ya
kupata kura 3,553 akifuatiwa na Joseph Kahungwa, kura 3,647 na Raphael Shilatu
(kura 864).
Waraka huo ambao
ulioandikwa Agosti 2, mwaka huu na kusainiwa na wagombea hao, unaeleza uchaguzi
huo wa kura za maoni katika jimbo hilo, uligubikwa na vitendo vya rushwa,
ulaghai, dhuluma na ukiukwaji wa taratibu na kanuni za uchaguzi.
Hata hivyo malalamiko hayo yameelekezwa kwa Katibu wa
CCM Wilaya ya Nyamagana, Elias Mpanda na Mabula ( Diwani wa Kata ya
Mkolani), aliyemaliza muda wake Julai 8, mwaka huu.
Waraka huo umeandikwa na
wagombea 10 kama yanavyosomeka hapo ni Stephen Deya, Robert Masunya, Raphael
Shillatu, Joseph Kahungwa, Tumaini Lusenga, Wisandara Muhindi, Komanya Kitwala,
Dede Petro, Aviasi Said na Tausi Halili..
Pia wagombea hao wanadai
na kumtuhumu Katibu huyo wa CCM wa
Nyamagana kwamba alitumia lugha kali na vitisho vilivyowanyima wao fursa na
uhuru wa kujieleza kwa wapiga kura na kumpatia muda mwingi wa kujieleza.
Wanadaiwa kuwa baadhi ya
wapiga kura walikutwa na kadi bandia ambazo walizikabidhiwa kwa katibu huyo
ambaye hata hivyo inadaiwa hakuchukua hatua zozote dhidi ya wahusika.
Kwa mujibu wa wagombea
hao, madaftari mengi kwenye matawi yalikuwa na majina ya wanachama wapya pekee,
huku wa zamini majina yao yakiwa hayaonekani ,hali iliyosababisha wanachama wa
muda mrefu kupinga uchaguzi huo katika baadhi ya vituo baada ya kunyimwa fursa
na haki ya kupiga kura.
Matawi yaliyokuwa na
tatizo hilo ni Maswa Magharibi, Isagenghe, Unguja, Ndofe, Nyamagana,
Mwananchi – Tandabui na Nyakabungo, wengi wa wanachama wakiwamo wajumbe
wa mashina ( mabalozi), wenyeviti wa mtaa na baadhi ya wagombea udiwani majina
yao hayakuonekana kwenye vitabu, hivyo kunyimwa fursa ya kupiga kura.
“Vituo viwili
vilivyorudiwa uchaguzi vilifungwa mapema, ambavyo ni Isagenghe kilichofungwa
saa 8:00 mchana na Maswa Magharibi kilichofungwa saa 7:30 mchana.Licha ya
kuridiwa kwa uvhaguzi,hatukishirikishwa,”
“Uchaguzi katika matawi
ya Isagenghe na Maswa Magharibi uliahirishwa na kisha kufanyika siku iliyofuata
Jumapili Agosti 2/8/2015 bila wagombea kupewa taarifa na hii imefanyika ili
kutoa mwanya kupigwa kwa kura isivyo halali bila mawakala wa wagombea kuwapo
vituoni.
“Tumeshuhudia watu
wanakuja kupiga kura wakiwa na maelekezo ya kumpigia mgombea ndugu Mabula
kutoka kwa mwanachama aliyekiri kuwa ni mtu wa Mabula,” inaeleza sehemu ya
waraka huo ( nakala yake tunayo)
Malalamiko mengine
yanaeleza kwamba lilikuwapo kundi la vijana wenye umri wa chini ya miaka 14
walioandaliwa kumpigia kura Mabula kwa kutumia kadi za CCM kutoka jimbo jirani
la Ilemela.
Inadaiwa katika warka
huo kuwa, mmoja wa vijana hao amekiri kumpigia kura Mabula kwa kadi hiyo ambyo
imetumika zaidi ya mara moja katika kituo kile kile cha Isagenghe. Kadi hiyo ni
namba AF 5590765 iliyotolewa tarehe 25/10/200.
Kuhusu rushwa, wanadai
wana ushahidi wa kuthibitisha jinsi Mabula alivyogawa fedha kwa vijana 30 ili
wampigie kura ya maoni na baadhi yao waliruhusiwa kupiga kura bila kuwa
na kadi za chama,pia alitumia gari T.151 DAY aina ya Noah,kugawa rushwa kwa
wapiga kura, iliyopewa jina la gari la BOT.
“Mkurugenzi wa Uchaguzi
ambaye ni Katibu wa Wilaya (Mpanda) ameonyesha upendeleo kwa ndugu Mabula tangu
kipindi cha kampeni na upigaji wa kura za maoni kwani alionekana kupewa
upendeleo wa muda wa kutosha kujinadi kuliko mgombea yeyote.
“Kwa misingi hiyo,
hatukubaliani na matokeo hayo na hatuungi mkono juhudi zozote za kumpitisha
Mabula aliyeonekana kuhujumu maslahi mapana ya chama na kuharibu mshikamano wa
wagombea wenzie na wanachama kwa ujumla.
“Ombi letu, tunaomba
busara za chama zitumike ili kukomboa jimbo letu kutoka kwa wapinzani kwa
kupata mgombea safi asiyekuwa na wasifu wenye madoa, anayekubalika ndani na nje
ya chama,” wanaeleza wagombea hao katika waraka huo.
Juhudi za kumpata Mabula
ili kuzungumzia sakata hilo, hazikuzaa matunda baada ya gazeti hili kumpigia
simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa na mara nyingine haikupatikana.
Katibu wa CCM Wilaya ya
Nyamagana, Elias Mpanda, juhudi za kumpata kiongozi huyo kujibu malalamiko hayo
licha ya mwandishi wa habari hizi kwenda ofisini kwake hakumkuta hata
alipopigiwa simu yake ya mkononi haikuwa hewani.
Katibu wa CCM Mkoa wa
Mwanza, Miraji Mtaturu, alipoulizwa
alikiri kupokea malalamiko ya wagombea hao wanaopinga matokeo ya kura ya maoni
ya ubunge katika Jimbo la Nyamagana na kuongeza kuwa karibu matokeo katika
majimbo yote ya mkoa wa Mwanza yamelalamikiwa.
“Malalamiko hayo si
Nyamagana pekee, kuna, Ilemela, Magu na Kwimba yote yanalalamikiwa,Watu wanajenga
dhana kuwa wanaposhindwa wanalalamika kuwa hawakutendewa haki,” alisema
Mtaturu.
Mtaturu alisema ofisi
yake haiwezi kuzuia mamlaka ya juu ya chama hicho na Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) kuendelea na mchakato wa kupitia na kuthibitisha majina ya wagombea
ubunge hadi hapo itakapojiridhisha kuwa malalamiko hayo ni kweli.
mwisho